1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo
Matangazo
Matangazo

Habari

Habari za Ulimwengu | 22.01.2021 | 03:00

Biden aagiza kuvaliwa kwa barakoa, sheria mpya za usafiri dhidi ya corona

Rais wa Marekani Joe Biden ametilia mkazo sheria za kuvaa barakoa na kuagiza kuwekwa chini ya karantini kwa watu wanaosafiri kuelekea nchini humo wakati akianza kutekeleza majukumu yake katika kukabiliana na janga la virusi vya corona katika siku ya kwanza madarakani. Akitia saini maagizo 10 ya rais katika ikulu ya White House, Biden ameliambia taifa hilo kwamba idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19 huenda ikaongezeka hadi nusu milioni kufikia mwezi ujao na kwamba hatua za dharura zinahitajika.Biden amesema kuwa taifa hilo liko katika hali ya dharura na ni wakati wa kuichukulia hali nchini humo kuwa hivyo. Ameongeza kwamba anataka kurejesha imani ya umma baada ya utawala wa mgawanyiko wa Donald Trump. Biden amesema kwamba chini ya utawala wake, wanasayansi watafanya kazi bila kuingiliwa kisiasa na kuahidi kushauriana nao kila wanapokosea.

Viongozi wa EU wahimiza watu kupunguza safari kudhibiti corona

Viongozi wa Umoja wa Ulaya jana waliwataka raia wa bara hilo kutosafiri kiholela na kuonya kuwa hatua kali za vizuizi dhidi ya safari zinaweza kuchukuliwa katika siku zijazo iwapo juhudi za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona zitashindwa. Viongozi wa Umoja huo Ursula Von der Leyen na Charles Michel walitoa onyo hilo baada ya mkutano wa saa nne ulioandaliwa kwa njia ya video na kujumuisha viongozi wa mataifa 27 ya Umoja huo ulioangazia hatua za kukabiliana na wimbi la pili la janga hilo la corona.Hatua hiyo inachochewa na hofu ya kuenea kwa aina mpya ya virusi hivyo vinavyoambukiza zaidi ambavyo huenda vikasababisha kuongezeka kwa idadi ya maambukizi ambayo tayari iko juu na kutatiza huduma za matibabu katika hospitali kama inavyoshuhudiwa nchini Uingereza. Viongozi hao wawili waliongeza kuwa utaratibu zaidi juu ya suala hilo utachukuliwa katika siku zijazo.

Merkel na EU wasisitiza kuachiliwa kwa Navalny

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Umoja wa Ulaya, Jana walisisitiza wito wa kuachiwa huru kwa kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny aliyekamatwa katika uwanja wa ndege wa Moscow wiki iliyopita alipowasili kutoka Ujerumani. Akiwa mjini Berlin, Merkel amesema kuwa wanaamini kuwa hatua hiyo ndio ya haki na dharura. Rais wa Finland Sauli Niinisto pia aliibua swali hilo wakati wa mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin. Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Niinisto, rais huyo alizungumzia kuhusu athari za kuzuiliwa kwa Navalny katika uhusiano wa mataifa ya Ulaya na Urusi. Kufuatia mkutano kwa njia ya video, Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel amelaani hatua ya kuzuiwa kwa Navalny na kutoa wito wa haki zake kuheshimiwa kikamilifu.

Mashambulizi ya mabomu nchini Iraq yasababisha vifo vya watu 32

Mashambulizi mawili ya mabomu ya kujitoa mhanga yamefanyika katika soko lenye shughuli nyingi katika mji mkuu wa Iraq hapo jana na kusababisha vifo vya takriban watu 32.Mamlaka nchini humo inasema kuwa hili ni tukio la kwanza kubwa la shambulizi la mabomu katika muda wa miaka mingi na kuirejesha nchi hiyo nyuma katika siku za mashambulizi ya mara kwa mara ya wanamgambo. Shambulizi hilo la nadra la kujitoa mhanga lilitokea katika eneo la kibiashara la Bab al-Sharqi katikati mwa Baghdad huku kukiwa na mvutano mkubwa wa kisiasa kuhusu mipango ya uchaguzi wa mapema na mgogoro mkubwa wa kiuchumi. Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo, lakini maafisa wa jeshi la Iraq wanasema ni kazi ya kundi linalojiita Islamic State, IS.

CAR yatangaza hali ya hatari huku waasi wakivamia mji mkuu

Jamuhuri ya Afrika ya Kati Alhamisi ilitangaza hali ya hatari ya siku 15 kufuatia jaribio la makundi yenye silaha kuuzingira mji Bangui katika juhudi za kumwondoa mamlakani Rais aliyechaguliwa tena Faustin Archange Touadera. Katika tangazo kupitia redio ya taifa, msemaji wa ofisi ya rais Albert Yaloke Mokpeme amesema kuwa hali hiyo ya hatari imetangazwa kote nchini humo kuanzia saa sita usiku. Mokpeme ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba hali hiyo ya hatari pia itaruhusu mamlaka ''kukamata watu bila kupitia waendeshaji mashtaka wa kitaifa.'' Tamko hilo la Alhamisi limekuja saa chache baada ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo kulitaka Baraza la Usalama kukubali "ongezeko kubwa" la idadi ya wanajeshi wa kudumisha amani nchini humo kukabiliana na ghasia mbaya.

UN yaidhinisha kongamano la kimataifa kuhusu ulinzi wa maeneo ya kidini

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kulaani uharibifu wa maeneo ya kidini na kumtaka katibu mkuu wake kuandaa kongamano la kimataifa kuongoza katika uungwaji mkono wa umma katika kulinda maeneo ya urithi wa kidini. Azimio hilo lilipendekezwa na Saudi Arabia na kufadhiliwa na mataifa ya Kiarabu yanayozijumuisha Misri, Iraq, Jordan, Kuwait, Yemen, Bahrain, Sudan, Oman, Muungano wa Falme za Kiarabu na Palestina, ambayo inatambuliwa na Umoja wa Mataifa kama taifa mwangalizi. Bangladesh, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mauritania, Morocco, Nigeria, Pakistan, Ufilipino na Venezuela pia zilikuwa wadhamini wenza. Azimio hilo linalaani kuongezeka kwa mashambulizi ya mali za kitamaduni ikiwa ni pamoja na maeneo ya kidini na vitu vya kitamaduni yanayofanywa na makundi ya wanamgambo na mara nyingi kusababisha uharibifu, wizi na uuzaji wa bidhaa zilizoibwa.

Wanajeshi watano wauawa katika operesheni dhidi ya magaidi Niger

Wizara ya ulinzi ya Níger imesema jana kuwa wanajeshi watano wa Nigeria wameuawa na wanne hawajulikani walipo, kufuatia operesheni dhidi ya kundi la itikadi kali katika eneo la Kusini Mashariki mwa nchi hiyo katika mpaka wake na Nigeria. Katika taarifa kupitia televisheni, wizara hiyo imesema kuwa ''takriban magaidi 20'' pia waliuawa katika mapigano hayo ya siku ya Jumanne. Hata hivyo haikutoa maelezo kuhusu operesheni hiyo dhidi ya kundi hilo la itikadi kali mbali na habari kwamba iliungwa mkono na ''washirika'' wa Niger na kupelekwa kwa vikosi vya jeshi la anga na ardhini. Niamey ni sehemu ya muungano wa mataifa yanayoungwa mkono na Ufaransa katika eneo la Sahel yanayopambana na wanamgambo wa itikadi kali ikiwa ni pamoja na wengine wa kundi linalofungamana na lile linalojiita Islamic State linalojuliakan kama ISWAP lenyewe likiwa tawi la Boko Haram.

Matukio ya kisiasa

Matukio ya Afrika

Masuala ya jamii

Michezo

Habari kwa lugha ya Kiingereza

Redaktionsfoto Kisuaheli

Bonyeza hapa kupata Matangazo na ripoti zetu

Matangazo
Tazama vidio 02:41